KILIO CHA WAKAZI WA TASIA KUHUSU MAFUTA

Wakazi wa eneo la Tassia wameendelea kubaki majumbani huku mgomo wa usafiri kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ukiingia siku ya pili. Hali hiyo imesababisha shughuli nyingi kusimama huku magari ya matatu na boda boda nyingi zikikosa kufanya kazi katika eneo hilo.

Akizungumza na Koch FM, mfanyabiashara wa mboga Charity Maina amesema hali imekuwa ngumu sana kwake kwani hawezi kusafiri kwenda sokoni mjini kuchukua mboga mpya za kuuza.

“Biashara imekuwa ngumu sana. Hakuna usafiri wa kutupeleka town kuchukua mboga mpya na hata wateja wamepungua kwa sababu wengi wamebaki nyumbani,” alisema Charity.

Douglas ambaye ni dereva wa boda boda katika eneo hilo alisema waendeshaji wengi wamelazimika kujiunga na mgomo huo baada ya wateja kukataa kuongezwa nauli kutokana na gharama ya mafuta.

“Bei ya mafuta iko juu sana. Tukiongeza bei ya safari wateja wanakataa, hivyo tumeamua kusimamisha kazi hadi serikali itupatie suluhisho,” alisema Douglas.

Kwa upande wake Mohammad, mkazi wa Tassia, amesema hatawaruhusu watoto wake kwenda shule hadi serikali itakapochukua hatua kuhusu bei ya mafuta na gharama ya maisha.

“Hakuna usafiri na maisha imekuwa ghali sana. Serikali lazima itusikize kwanza kabla watoto warudi shule,” alisema Mohammad.

Wakazi sasa wanaendelea kuitaka serikali kushusha bei ya mafuta na kupunguza gharama ya maisha ili shughuli za kawaida ziweze kurejea katika maeneo ya Tassia na maeneo ya karibu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top